Suala la mshambuliaji Mbwana Samatta kuwa njiani kutua kwenye klabu ya AS Roma ya Italia, limechukua nafasi kubwa katika mitandao ya kijamii tangu asubuhi ya hii leo, na kuzua maswali mengi miongoni mwa mashabiki wa soka nchini Tanzania.

Samatta alisajiliwa na klabu ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji, mwezi Januari mwaka huu na uhamisho wake ulikua wazi na ulimfurahisha kila mpenda soka hapa nchini, lakini suala la kuelekea AS Roma limekua la ghafla na kugubikwa na usiri mkubwa.

Kutokana na hali hiyo, chanzo kimefanya mazungumzo na meneja wa mshambuliaji huyo ambaye kabla ya kutimkia nchini Ubelgiji alikua akicheza soka la kulipwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, katika klabu ya TP Mazembe ambayo aliisaidia kutwaa ubingwa wa Afrika mwaka 2015.

Jamal Kisongo ambaye ni meneja na mlezi wa Samatta, amesema hakuna lolote kuhusiana na hilo na Samatta anaendelea na maandalizi katika kikosi chake cha KRC Genk kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Ubelgiji.

“Nimesikia pia, kuna watu kadhaa wameniuliza pia. Lakini ukweli ni hivi; Mbwana anaendelea na maandalizi ya Ligi Kuu Ubelgiji.

“Hakuna lolote kuhusiana na Roma hadi sasa labda kama litakuja baadaye. Mawakala wake wote wanalijua hilo.

“Timu haiwezi ikafanya mawasiliano ya kumuuza bila ya kuwaeleza mawakala wake, meneja wake. Ndiyo maana nasema labda suala hilo lije baadaye,” alisema Kisongo.

Advertisements