Jay Moe amenukuliwa mara kibao akidai kuwa katika nyimbo zake zote alizowahi kufanya, Famous ni wimbo uliopotea bila kuwa na video. Wimbo huo ulitoka mwishoni mwa mwaka 2011 na ulikuwa ujio wake mpya enzi hizi baada ya kukaa kimya tena kiaina.

Kwangu mimi, Famous si tu miongoni mwa ngoma kali za muda wote za Jay Moe, bali za hip hop ya Tanzania. Ni wimbo wenye beat kali, chorus inayoshika masikioni na kila neno alilorap Moe linawakilisha maisha ya mastaa wote duniani.

Ni wimbo mwingine pia uliodhihirisha kuwa Majani si producer mkali tu bali muimbaji mzuri wa viitikio pia. Majani aliweka moja ya chorus tamu nilizowahi kuzisikia kwenye muziki wa Bongo.

Famous ulikuwa wimbo mkubwa mno na pengine ulimwogopesha hata Jay Moe kufanya video yake wakati huo kwa kuogopa kupata isiyo na kiwango. Na hakika ni vyema kutofanya video kabisa kuliko kufanya video mbovu kwa ngoma kali.

Miaka mitano imepita, masikioni mwangu nausikiliza wimbo huo kwa sauti ya juu lakini nausikia kama umetoka jana tu. Famous bado ni wimbo mtamu, mkali na unazitoa knock out ngoma kibao zilizotoka miaka mingi baada yake. Wanasema cha zamani ni dhahabu lakini Famous imepitiliza – ni almasi kabisa.

Ni wimbo uliodhihirisha kwa mara nyingine tena kuwa Jay Moe ni rapper mkali kuwahi kutokea kwenye ardhi ya Tanzania.

“Bado ukipigwa hadi leo unasound kisasa zaidi tofauti na kama nikisema nataka kushoot ‘Kama Unataka Demu’ kuna wengine siwezi kuwapata kirahisi, lakini Famous it’s just me and P-Funk na kuonesha tu hiyo lifestyle ya famous guy inakuaje, kwahiyo tunataka tushoot hiyo,” Jay Moe aliiambia 255 kwenye kipindi cha XXL cha Clouds FM.

Lakini mimi nadhani kuipa video yake pekee haitoshi – hiyo itakuwa ni kama kuweka sukari kwenye jojo iliyoisha utamu. Kuna ulazima wa Jay Moe kuipa upya ngoma hii. Na upya wenyewe si wa kuandika verse mpya, bali ni kwa kuongeza rappers wengine kutengeneza bidhaa mpya yenye nguvu zaidi. Beat na chorus zibaki vile kwa sababu siamini kama kuna namna ya kutengeneza mpya za kuzidi ukali wa zile za mwanzo.

Imagine Mwana FA akaingiza verse yake kuelezea tafsiri yake ya umaarufu. Imagine Fid Q aliyewahi kusema ‘usupastaa ni mzigo wa mwiba’ akieleza experience yake ya kuwa maarufu Bongo. Pata picha Chidi Benz akiingia naye kusema ya upande wake. Fikiria Profesa Jay, Mr Blue na rappers wengine wakiirukia ngoma hiyo! Jay Moe atakuwa na kitu kikubwa mkononi mwake ambacho kikiwa na video yake kitaonesha jinsi ambavyo Tanzania imebarikiwa kuwa na wachanaji wakali.

Advertisements