shilole (2)
 
DAR ES SALAAM: Mtiti! Msanii nyota wa Muziki wa Kizazi Kipya, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ wikiendi iliyopita alitoa kali ya mwaka, baada ya kuzichapa kavukavu na mlinzi ‘baunsa’ wa pool party yake iliyofanyika katika eneo la ofisi ya BKT iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam, baada ya kumfanyia ‘kauzibe’.

shilole (1)
ILIVYOKUWA AWALI
Shilole, ambaye ni balozi wa kondomu zinazofahamika kama Bulls Mpe Raha, alikuwa amefanyiwa sherehe na kampuni inayosambaza bidhaa hiyo ili aburudike yeye pamoja na watu wake wa karibu, sambamba na wadau wengine wa ‘menejimenti’ hiyo.
Kama mtu mwenye shughuli, msanii huyo anayejisifu kwa uamuzi wake wa kutoka na ‘vijana wadogo’, aliwaalika baadhi ya watu wake wa karibu, wakiwemo wasanii wenzake na kuifanya pati hiyo kuwa yenye kuvutia, kwani vyakula na vinywaji halikuwa jambo la kuuliza.
shilole (3)
ATAKA KUONDOKA KUWAHI BILLS
Ilipofika saa saba za usiku, Shilole alitaka kuondoka kwenye pati hiyo ili awahi katika shoo, ambayo alitakiwa kuifanya katika Ukumbi wa Billicanas uliopo katikati ya jiji, yeye na Vanessa Mdee ‘Vee Money’.
Lakini kwa vile vinywaji vilikuwa bado vingi na yeye hakuwa ametosheka, alimuomba mtu aliyeonekana bosi wa kampuni hiyo, aruhusiwe kubeba bia zisizohitajika kurejesha chupa (take away), kitu ambacho kilikubalika na mkali huyo wa Kibao cha Nyang’anyang’a akajisevia chupa zipatazo kumi za bia za bei mbaya tayari kwa kusema.
AKUTANA NA BAUNSA GETINI
Getini, staa huyo ambaye pia anajulikana kama Shishi Baby, akakutana na baunsa aliyetoa maneno ambayo Shilole alitafsiri kama yenye kumdhalilisha.
“Hamna kutoka na bia hapa, watu wote tumewazuia kuondoka na bia, kwani wewe ni nani hasa, hizo chupa kesho tuna kazi ya kuzihesabu,” alisema baunsa huyo.
Shilole akiwa amepigwa na butwaa, alijitahidi kumuelewesha kistaarabu sababu za yeye kuchukua bia.
“Sikia kaka, hii shughuli ni yangu, watu wote hapa wamekuja kwa sababu yangu na isitoshe, hizi ni take away (chupa zisizohitajika kurudishwa), halafu pia nimemuomba meneja na ameniruhusu, wewe nani unanizuia?”
Baunsa huyo aliyefahamika kwa jina moja la Mansuri, hakuelewa somo, akashikilia msimamo wake, licha ya baadhi ya wadau walioanza kukusanyika, kumsihi atumie busara.
HALI YA HEWA YACHAFUKA, PACHIMBIKA
Baada ya Shilole kuona ‘saundi’ zake hazina msaada, akaamua kujilipua, liwalo na liwe kwa kuanzisha vurugu akilazimisha kutoka na vinywaji vyake, jambo lililosababisha wawili hao kuchapana vibao.
Wadau waliokuwa karibu na tukio hilo walisogea na kutaka kuingilia kati, lakini Shilole alikuwa mkali, jambo lililosababisha wasamaria wema hao kupata wakati mgumu kuwaamulia.
Hata hivyo, baadaye walifanikiwa kuamua ugomvi huo, uliomuacha Shilole akiwa hoi kwa uchovu uliochanganyika na kinywaji.
SHILOLE ALONGA
Baada ya timbwili hilo, msanii huyo alionesha mshangao wake kwa mlinzi huyo, baada ya kuliambia gazeti hili kuwa ni jambo la kushangaza kuona mtu ambaye hafahamu umuhimu wake katika kampuni anayoitangaza, kumzuia kuondoka na bia.
“Mimi ndiyo mara yangu ya kwanza kuwa balozi na nimeanza kazi vizuri, nashangaa mtu anataka kuniharibia wakati hata hahusiki, hawa watu wote hapa nimewaalika mimi, leo mtu haoni.
“Hata kama chupa zile zinahesabiwa kesho yake, kwani si angesema nilichukua mimi, kulikuwa na tatizo gani?” alisema.