Waziri Mkuu wa Uingereza amewaomba vijana wa nchi hiyo waunge mkono nchi hiyo kusalia katika uanachama wa Umoja wa Ulaya katika kura ya maoni iliyopangwa kufanyika tarehe 23 mwezi Juni.

David Cameron amewaomba vijana wa Uingereza washiriki kwenye kura hiyo ya maoni kwa kupiga kura ya ndio na hivyo kupinga kuondoka Uingereza katika Umoja wa Ulaya. Waziri Mkuu wa Uingereza ametahadharisha kuwa kuondoka Uingereza katika Umoja wa Ulaya kutasababisha madhara mengi kwa vijana wa nchi hiyo.

Katika hali ambayo chunguzi za maoni zilizofanyika Uingereza zinaonyesha kuwa kuna hitilafu kubwa za maoni na kimitazamo kati ya wale wanaounga mkono kuendelea unachama wa nchi hiyo katika EU na wale wanaopinga suala hilo, inaonekana kuwa vijana wa Uingereza watakuwa na nafasi muhimu katika matokeo ya kura hiyo ya maoni.

Shirika la habari la Reuters katika uchambuzi wake limeongeza kuwa, tafiti mbalimbali za maoni zinaonyesha kuwa kwa kiasi kikubwa vijana nchini Uingereza wanaunga mkono nchi hiyo iendelee kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, hata hivyo vijana hao hawaonekani kuwa na shauku kubwa ya kushiriki katika kura hiyo ya maoni.